TOP

PAGE 10

I Previous page I Full page List I Next page

Utenzi wa Shaaban Robert. :

Poems by Shaaban Robert

photoshaaban

I. Utenzi wa Hati

  1. Leo nataka binti,
    Ukae juu ya kiti,
    Ili uandike hati,
    Ndogo ya wasia

  2. Mimi kwako ni baba,
    Hati hii ya huba,
    Andika iwe akiba,
    Asaa itakufaa.

  3. Bado ungali kijana
    Na dunia ngumu sana,
    Kukufunza kukuona,
    Ni jambo welekea.

  4. Kwa faidayo mtoto,
    Kwanza andika vito,
    Vya kima na uzito,
    Ufananishe tabia.

  5. Ulimwengu una adha,
    Njiaze kadha wa kadha,
    Itunze kama fedha,
    Hati utabrikiwa.

  6. Dunia ina aibu,
    Hati hii ni dhahabu,
    Tunza kama sahibu,
    Itakupa manufaa.

  7. Usifanye tashititi,
    Na watu kuwasaliti,
    Hati hii ni yakuti,
    Nakupa kama hidaya.

  8. Kama utaikariri,
    Hati na kuifikiri,
    Utaona ni johari,
    Ndipo hakutunukia.

  9. Hati iwe zumaridi,
    Katika yako fuadi,
    Ambaa na ufisadi,
    Utiao utu doa.

  10. Hati hii ni lulu,
    Iweke utafaulu,
    Wema huwatahulu,
    Baraka kukuombea.

  11. Kuombewa njema dua,
    Mtu hujaliwa,
    Siri kuzitambua,
    Na heri kumfikia.

  12. Aombewaye laana,
    Dua zikizidi sana,
    Wokovu huwa hana,
    Ila kuangamia.

  13. Mungu hutia kabuli,
    Katika zetu kauli,
    Maamuzi ya kweli,
    Ndiye anayetoa.

  14. Na sauti nyembamba,
    Hupaa kama kwamba,
    Kwa mbawa zimepambwa,
    Kwenda tusikojua.

  15. Hasa imethibitika,
    Kabisa bila shaka,
    Neno likitamkwa,
    Katika hewa hupaa.

  16. Hupaa hata ng'ambo,
    Aliko Mwelewa mambo,
    Wala hapana jambo,
    Yeye asilosikia.

  17. Hati haya isemayo,
    Fananisha na radio,
    Sauti yendavyo mbio,
    Toka mbali kukujia.

  18. Hati hii muktasi,
    Tunza kama almasi,
    Jihadhari na matusi,
    Kinywa ovyo kutoa.

  19. Tena uwe azizi,
    Kila unapobarizi,
    Hati hii ni feruzi,
    Kama utaangalia.

  20. Dunia ni mvurugo,
    Japo hati ni ndogo,
    Ukiitunza mitego,
    Mibaya utaambaa.

  21. Hati usione nzito,
    Nakupa huba mtoto,
    Itakuletea pato,
    Mwangaza wa dunia.

  22. Mtoto ishiketo,
    Cheche huzaa moto,
    Mto huanza kijito,
    Tone bahari na ziwa.

  23. Weka na kuihifadhi,
    Kwako iwe kama radhi,
    Mambo ya hii ardhi,
    Watu wengi husumbua.

  24. Hati hii ni mali,
    Kwa mtu wa akili,
    Ifanye kama kipuli,
    Siku ya kujikwatua.

  25. Fanya kama kipini,
    Bora hakina kifani,
    Itaongeza uoni,
    Hati ukishikilia.

  26. Nakupa iwe hereni,
    Pambo la masikioni,
    Hati iweke moyoni,
    Siku moja itafaa.

  27. Shikamana na ibada,
    Kutimiza kila muda,
    Na kesho ina faida,
    Ikisha hii dunia.

  28. Dini mali ya roho,
    Mwilini kama joho,
    Unapoteza uroho,
    Na anasa za dunia.

  29. Hati hii ni ya nuru,
    Shika nakuamru,
    Mungu atakunusuru,
    Akuepushe na baa.

  30. Back to Top

  31. Jifunze na elimu,
    Uwe mtu taalamu,
    Halali na haramu,
    Uweze kupambanua.

  32. Elimu kitu kizuri,
    Kuwa nayo na fahari,
    Sababu humshauri,
    Mtu la kutumia.

  33. Hati nakupa kafara,
    Weka na kitu bora,
    Utaokoka madhara,
    Na mengi udhia.

  34. Upishi mwema kujua,
    Na mume kumridhia,
    Neno analokwambia,
    Kwako itakuwa taa.

  35. Na mume msishindane,
    Wala msinuniane,
    Jitahidi mpatane,
    Ndiyo maisha ya ndoa.

  36. Fanya kila hali,
    La mume kulikubali,
    Ila lisilo halali,
    Kukataa si hatia.

  37. Nyumba yako inadhifu,
    Kwa kufagia uchafu,
    Kila mdudu dhaifu,
    Asipate pa kukaa.

  38. Ziko nyingine amali,
    Kujifunza ni halali,
    Taabu zikikabili,
    Uwe umejiandaa.

  39. Zikikukuta tayari,
    Taabu hazihasiri,
    Wala huwezi kukiri,
    Kukushawishi vibaya.

  40. Taabu zikikukuta,
    Waweza nazo kuteta,
    Njia ya kupita,
    Lazima zitakwachia.

  41. Lakini zikikuona,
    Huwezi nazo pigana,
    Zitakusumbua sana,
    Hati hii yafunua.

  42. Tia katika moyo,
    Nia ya maendeleo,
    Hatio hii ni cheo
    Kushinda ovu andaa.

  43. Maovu yanavizia,
    Na mtu kujiandaa,
    Kuweza kuyazuia,
    Tuzo bora hupewa.

  44. Hati nakupa ngao,
    Ndiyo usiseme siyo,
    Siyo ukasema ndiyo,
    Kubatilisha vibaya.

  45. Kutumika ni sharti
    Wajibu kila binti,
    Usingoje bahati,
    Yote kukutendea.

  46. Watu wengi huchelewa,
    Kwa kungoja kutendewa,
    Bahati wakaambua,
    Zingatia sana haya.

  47. Wakati tanabahi,
    Mtu sharti kuuwahi,
    Lakini kuusihi,
    Kungoja ni kupotea.

  48. Wakati huteleza,
    Una nuru na giza,
    Wapo wanaopoteza,
    Kwa kungojeangojea.

  49. Hati unayopewa,
    Kama utafanya nia,
    Daima kushikilia,
    Huzami utaelea.

  50. Majivuno hayafai,
    Yaleta uadui,
    Japo mtu humjui,
    Kumdunisha hatia.

  51. Usishiriki uongo,
    Ijara upate hongo,
    Mtu mwongo ni msungo,
    Masuto mengi hupewa.

  52. Masuto si mazuri,
    Yanapunguza kadiri,
    Jitihadi kujibari,
    Mbali na kila doa.

  53. Jambo usiloliona,
    Haifai kunong'ona,
    Hiyo ndiyo fitina,
    Mngwana ya kujitoa.

  54. Ulimi kulainisha,
    Neno likafurahisha,
    Ni furaha ya maisha,
    Kila wakati tumia.

  55. Ulimi wa pilipili,
    Hutenga watu wawili,
    Kuishi mbalimbali,
    Hii hasara sikia.

  56. Ulimi ulio tamu,
    Hupendeza wanadamu,
    Cheko na tabasamu,
    Unalosema hupewa.

  57. Hupendeza wasikizi,
    Wakati wa maongezi,
    Hili ni jambo azizi,
    Wajibu kuliania.

  58. Ulimi mzuri mali,
    Huvuta walio mbali,
    Kusikiliza kauli,
    Namna unavyotoa.

  59. Tena nakupa fununu,
    Sikiliza sana nunu,
    Kila lililo tunu,
    Kulipata fanya nia.

  60. Usoni kuwa na haya,
    Juu ya jema na baya,
    Na akili ya kutua,
    Pambo katika dunia.

  61. Mawili haya ghali,
    Kukosa usikubali,
    Joharize mtu mbili,
    Ni akili na haya.

  62. Hizi ni tunu thabiti,
    Ashikaye madhubuti,
    Hakosi kupata kiti,
    Cha heshima kukalia.

  63. Hati yasema kwamba,
    Mwanamke zampamba,
    Nje na katika nyumba,
    Akiwa azitumia.

  64. Ujitenge na kutu,
    Inayoharibu utu,
    Mwanamke hawi kitu.
    Aibu akiingia.

  65. Mke ni nguo nyeupe,
    Doa katika utepe,
    Jihadhari usiipe,
    Haihimili madoa.

  66. Kupenda watukufu,
    Kwa kumilki sarafu,
    Na fukara kukashifu,
    Hati yasema vibaya.

  67. Penda wenye cheo,
    Na wanyonge uwe nayo,
    Hayo ndiyo mapokeo,
    Mema mtu kutumia.

  68. Kila mtu msharifu,
    Dunia ni badilifu,
    Shida sana kuarifu,
    Mtu atayekufaa.

  69. Mwema hujiharibu,
    Ikampasa adhabu,
    Na mbaya akitubu,
    Dhambi zake hufutiwa.

  70. Kitu cha bure heshima,
    Mpe baba na mama,
    Kila mtu mzima,
    Na walio nawe sawa.

  71. Ukosefu wa adabu,
    Ni jambo la aibu,
    Wajibu kujitanibu,
    Mbali nalo kukaa.

  72. Mpungufu wa adabu,
    Duniani ana taabu,
    Hakaribishwhi karibu,
    Marafiki humwambaa.

  73. Iweke moyoni hati,
    Ubora wake thabiti,
    Hapana tofauti,
    Heri itakujia.

  74. Tumbo la rutuba,
    Umepewa kama huba,
    Uzae mama na baba,
    Kustawishi dunia.

  75. Back to Top

  76. Tumbo hili la dhahabu,
    Huzaa wenye thawabu,
    Na wengine wa ajabu,
    Hupata kuzaliwa.

  77. Kwa hivi una uzazi,
    Kuuguza na ulezi,
    Hutaka maangalizi,
    Bora hati yakwambia.

  78. Tena kujitegemea,
    Ni ngao ya ukiwa,
    Siku ya kubakia,
    Peke yako hufaa.

  79. Peke yako ukiwa,
    Wajibu kukaza nia,
    Tendo likishirikiwa,
    Sifa yake hupungua.

  80. Sifa ya peke kubwa,
    Vigumu sana kuzibwa,
    Hata kama ikikabwa,
    Ushahidi itatoa.

  81. Sifa ya wengi shirika,
    Lazima kugawanyika,
    Ya peke joho huvika,
    Mmoja mteuliwa.

  82. Katika maisha yetu,
    Ana chango kila mtu,
    Japo kidogo si kitu,
    Toa unachojaliwa.

  83. Chango mbaya ni uvundo,
    Wajibu kutenga kando,
    Bora huacha uhondo,
    Daima hukumbukiwa.

  84. Tendo bora hudumu,
    Kufutika ni vigumu,
    Baya kwa wanadamu,
    Halina pa kukaa.

  85. Unmeikuta dunia,
    Vema imeandaliwa,
    Karim kukupokea,
    Shukurani zako toa.

  86. Umekuta wasafiri,
    Walioipa kwa heri,
    Wameiweka vizuri,
    Nawe zidisha sitiwa.

  87. Kukinai jifundishe,
    Kidogo kikutoshe,
    Kikubwa sijizoeshe,
    Kukujia kwa hatia.

  88. Pato lako la halali,
    Japo ni kitu dhalili,
    Ni bora kuliko mali,
    Fedheha inayotia.

  89. Hati fanya kikuba,
    Moyo wako utashiba,
    Dunia ina ghiliba,
    Kama hukuangalia.

  90. Hati hii ni kifuli,
    Kinga yako ya mwili,
    Shauku kitu batili,
    Kwa uzuri kuchafua.

  91. Uzuri wako wa sura,
    Kufanye uwe imara,
    Sharti uwe na busara,
    Ya kuambaa hadaa.

  92. Na ubaya wa sura,
    Unaweza kuwa bora,
    Kama unayi fikira,
    Ya matendo ya murua.

  93. Zamu moja twaishi,
    Ikisha haturudushwi,
    Maisha ya fawaishi,
    Acha kuandamia.

  94. Ewe binti tajiri,
    Siku zote jihadhari,
    Kutengana na kiburi,
    Mali huota mbawa.

  95. Na binti maskini,
    Usiache abadan,
    Kujizidisha thamani,
    Kwa kuwa mwaminiwa.

  96. Binti wa mkubwa,
    Watu usiite mbwa,
    Fahari inapozibwa,
    Nawe utasimbuliwa.

  97. Na binti wa mdogo,
    Waweza kupata togo,
    Kwa kufuata mwigo,
    Wa matendo ya murua.

  98. Hati nawapa wote,
    Tunzeni kama pete,
    Mazao mema mpate,
    Mfurahie dunia.

  99. Dunia jengo lake,
    La mume na mwanamke,
    Kazi hii mshike,
    Hata kufanikiwa.

  100. Ijengeni kwa tofali,
    Wote watu wawili,
    Hata iwe kamili,
    Iwardhishe kukaa.

  101. Kazi hii itendeke,
    Pasiwe na pekepeke,
    Wajao nyuma wacheke,
    Kuona imetimia.

  102. Wakatabahu beti,
    Mtenzi wa hii hati,
    Ni Shaaban Robert,
    Jina mwaarifiwa.

Back to Top

'Utenzi wa Hati' ulichapwa ndani ya kitabu cha Shaaban Robert, 'Maisha Yangu Na Baada Ya Miaka Hamsini',


Maisha yake :

Wazazi wa Shaaban Robert walikuwa kabila la Kiyao, lakini alijiita mwenyewe daima 'Mswahili'. Yeye alizaliwa tarehe 1 Januari, 1909 kijiji cha Vibambani jirani na Machui kilomita 10 kusini mwa mji wa Tanga, na alipata elimu yake katika shule ya Msimbazi, jijini Dar-es-salaam.

Akawa karani katika idara ya forodha huko Pangani mwaka 1926 – 1944. Tangu 1944 mpaka 1946 alikuwa katika ya Idara ya Wanyama, na baadaye, kutokea mwaka 1946 hata 1952 alifanya kazi Afisi ya Mkuu wa Jimbo la Tanga, na kutokea 1952 mpaka 1960 Afisi ya Kupima Nchi Tanga.

Alioa mara tatu, na alikuwa na watoto kumi, lakini alipofariki aliacha watoto watano.

Athari yake kubwa katika mwendeleo wa lugha ya Kiswahili ni kwa sababu, pamoja na maandiko yake, alikuwa mwanachama wa 'East Africa Swahili Committee', 'East Africa Literature Bureau' na 'Tanganyika Languages Board', na 'Tanga Township Authority'(baadaye 'Town Council').

Alifariki dunia tarere 22 Juni, 1962 na alizikwa Machui.

Kwa jumla Mzee Shaaban Robert aliandika vitabu ishirini na mbili. Baadhi ya vitabu hivi ni: Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika, Wasifu wa Siti Binti Saad, Baada ya Miaka Hamsini, na Maisha Yangu. Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha za Kichina, Kiingereza na Kirusi.

Back to Top

Shaaban Robert katika Wikipedia

I Previous page I Full page List I Next page

© M. E. Kudrati, 2006:This document may be reproduced and redistributed, but only in its entirety and with full acknowledgement of its source and authorship