Safari na vitendo vya Dom Francisco 1505 A.K / 910 A.H

TOP

PAGE 7b

Previous pageFull page ListNext page

Go to :Vasco de Gama - First voyage

Safari na vitendo vya Dom Francisco, Gavana ya Uhindi, katika maneno yaliyoandikwa juu ya meli ya 'Santa Rafael' ya Oporto, iliyoamriwa na Feman Suarez.

Kusoma na asili ya maandiko haya katika lugha ya kiingereza tumia kiungo Modern History Sourcebook

CONTENTS:YALIYOMO

  1. KILWA
  2. MOMBASA
  3. MALINDI

Katika mwaka wa 1505, tarehe ya Machi, 25, Jumanne, sikukuu kuwa uonyesho wa Bibi yetu, Dom Francisco d'Almeida alisafiri baharini pamoja na jumla ya meli ishirini. Kulikuwa manowari kubwa kumi na nne, na karaveli(1) sita. Walipita mzingo wa Rasi ya Taraja Zuri ya Afrika Kusini siku ya Juni, 20, na walichukuliwa mbali papo kiasi ya ligi(2) sabini. July, 2, kulikuwa dhoruba na radi, na watu wawili katika meli ya bendera , na mmoja juu ya 'Lyomarda' waliporomoka majini. Siki 18 ya Julai, waliona nchi mara ya kwanza, ligi 369 baada ya Rasi ya Taraja Zuri, karibu na Ylhas Darradeiras, ndipo ni ligi thelathini kutoka siwa ya Mozambiki. Na siku ya Julai 19, walifika upeo wa Mozambiki, hata Julai, 21, walipata kuvuka maji haba ya Sam Rafael, namo ni ligi thelathini kabla ya Kilwa.

KILWA

Jumanne, adhuhuri Julai 22, waliingia bandari ya Kilwa, pamoja na jumla meli nane. Mara moja, Kapitani-Mkuu Dom Franciso d'Almeida alituma Bona Ajuta Veneziano kumwita mfalme. Yeye alijiudhuru kutokuja, lakini badala yake alipeleka Kapitani-Mkuu zawadi zake ; Hizi zilikuwa mbuzi watano, ngombe mdogo, na nyingi za nazi na matunda mengine.

Siku ya pili, Kapitani-Mkuu alitoa amri meli zote ziwe tayari na mizinga. Halafu, makapitani, kila mmojawao kumevaa nguo zake hiari. na vifaa vyake kamili, alikwenda ndani ya chombo chake kukaa kando ya mji kutumaini mfalme ataazimu kutoka nje. Lakini Shehe Sultani alituma habari kwamba hataweza kuja naye alikuwa na wageni. Ingawa yatakiwa, ataipeleka hedaya ya Mfalme wa Ureno. Taarifa hiyo ililetwa na mamorisko(3 ) watano, waliokamatwa wakati ule ule.

Al fajri, Alhamisi, Julai 24, siku ya mkesha wa mtakatifu Mtume Yakubu, wote walikwenda pwani katika mashua zao. Ya kwanza kushuka nchini alikuwa Kapitani-Mkuu, na yeye alifuatwa na wengineo. Walikwenda moja kwa moja hata kasri ya mfalme, na njiani mamorisko wale tu ambao hawakupiga vita walisalimishwa na maisha yao. Kasrini, palikuwa mmorisko mmoja aliyekuwa dirishani pamoja na bendera ya Ureno mkononi, alikuwa akapiga sauti, "Ureno! Ureno! ". Bendera hiyo ilikuwa ile ilioachwa na Amir-l-bahr, Vasco da Gama wakati aliyekata shauri na Kilwa kutoa hedaya ya 1,500 wakia za dhahabu kila mwaka. Mmorisko aliambiwa afungue mlango na baada ya hakufanya hivyo mlango ulivunjwa na mashoka. Hawakuona tena yule mmorisko, wala mwowote mwingine ndani ya kasri, ambayo ilikuwa tupu.

Katika Kilwa kuna vyumba vyingi thabiti na vya urefu wa ghorofa nyingi. Vimejengwa hivi kwa jiwe na chokaa, na vimepakwa na lipu vya urembo mbali mbali. Mara mji ulichukuliwa bila ushindano, Kasisi-jamii na baadhi ya padre mafransisi walishuka nchini, mkononi wao walikuwa wameshika misalaba miwili, walikwenda mwandamano na kuimba 'Mungu wewe'. Walikwenda mpaka kasri, na pale msalaba uliteremshwa na Kapitani-Mkuu aliomba Mungu. Halafu, wote walianza kuteka nyara na kunyang'anya mali na mitaa yote ya mji.

Mji wa Kilwa upo juu ya kisiwa kinacho uwezo pande zote kuvukisha meli ya tani 500. Kisiwa na mji kuna jumla ya watu 4,000. Ni zazi sana, na inaleta mahindi ya aina kama yale ya Guinea, siagi, asali, na nta. Mizingi ya nyuki yatundika juu ya miti , kiasi ya vitungi vya 'almuda'(4) tatu, kila mmoja umefumwa na makuti. Kuna matundu yapitisha nyuki kwenda ndani na kutoka nje.

Hapo pana machungwa matamu, malimau, maboga, vitunguu vidogo na majani ya harufu. Yapandwa ndani ya bustani na yatiliwa maji ya visima. Hapo panapo mtambuu ambao una majani kama hedera(5), na hupandwa kama njegere kutegemea miti mzizini. Majani haya ya tumikwa na Waarabu wenye mali kutafuna pamoja na chokaa imeyotengenezwa kwa njia maalum kuonekana kama mpako. Waweka mbali yale majani hata kama yatapakwa juu ya majeraha. Majani haya yafanya meno na mdomo mekundu mno, lakini yasemwa kuwa kuburudisha sana.

Hapo, pana watumwa weusi zaidi kuliko mamorisko weupe : watumiwa kama walimaji wa mahindi na kadhalika shambani. Kuna aina za mibaazi ambayo inaletwa na miti mirefu kama miti mikubwa ya pilipili ; ingaliiva, yasanyikwa na kuwekea akiba. Ardhi ni nyekundu, na tabaka ya juu ndiyo ya mchanga ; majani ni daima rangi kijani kibichi. Kuna wanyama wengi wanono, ng'ombe maksai, ng'ombe, kondoo, mbuzi, na samaki tele; pia kuna nyangumi waogelea karibu na meli. Hamna maji kunywa ya mwendo kisiwani. Karibu ya kisiwa, kuna visiwa vidogo vyingine vimevyokaliwa na watu. Marekibu mengi yapo, ukubwa wa karaveli ya tani hamsini, na mengineyo madogo. Haya makubwa yalala pwani, na yakokotwa mpaka bahari ijapo watu wataka kuyachukua kwenda safari. Yajengwa bila misumari : mibao yashonwa pamoja na kumbi ya minazi limelofundwa. Kamba ya namna ileile inatumiwa katika usukani. Marekibu yapakwa na berua(6) nyeusi imeyotengenezwa na ubani na gundi. Yavuka bahari kutoka hapa mpaka Sofala, umbali wa ligi 255.

Minazi hapa haizai tende lakini kwa baadhi kwayo inatolewa divai na siki. Hivi ni vitokeo vya miti ya mivumo na hii haizai nazi. Nazi zina ukubwa wa matikiti makubwa, na makumbi ndani ya ganda, kwayo yatengenezwa kamba ya namna mbali mbali. Ndani ya kaka liko tunda kiasi ya ananasi kubwa. Humo, huwa painti nusu ya maziwa ambayo kunywa ni tamu sana. Baada ya kumaliza kunywa maziwa, nazi inavunjwa na inaliwa; kiini chake kuonja ni kama jozi(7) kabla ya kuiva. Wakausha kile, na hicho kinatoa kiasi kubwa ya mafuta.

Watu hapa walala juu ya ardhi katika machela imezotengenezwa na majani ya minazi, na hiyo hulalia mtu mmoja tu.

Wareno walivumbua kadiri kubwa ya maji yakunywa, Vyupa vya attari vyapelekwa nchi za nje kutoka hapa, pamoja na vioo vya aina mbali mabali, kila namna ya nguo za pamba, udi, sandarusi, dhahabu, fedha, na lulu. Kapitani-Mkuu alitoa amri kuhifadhia nyara ndani ya nyumba, fungwa na muhuri.

Ngome ya Kilwa ilijengwa huko kwa nyumba iliyokuwa bora zaidi kuliko nyingine. Na nyinginezo zilizokuwa karibuni yake zilibomolewa. Iliimarishwa, na mizinga ilitiliwa mahali yake pamoja na kila kitu kinachotakiwa bomani. Pero Ferreira aliachwa kuiamrisha na watu thamanini.

Nchi siyo joto sana. Watu wanao silaha za upindi na mishale mikubwa, vigao vigumu vya majani makuti yaliyofumwa na pamba, na mikuki iliyoukuwa mizuri zaidi kuliko ile ya Guini. Panga zilikuwa chache tu. Wanao teo nne zakutupa mawe lakini baado hawajui utumo wa baruti.

Bahari hulamba mwingizo wa ngome wakati wa kujaa maji karibu na pale panapo ingia meli.

Mfalme* alipotoroka kwa Kilwa, Kapitani-Mkuu alichagua mwingine , mmorisko mwenyeji aliyependezwa na wote, na ambaye walimwandamana juu ya farasi mpaka mwisho wa mji.

Chokaa inatengenezwa hapa kama hivyo: fungu la magogo ya miti linaviringishwa, na ndani yao yawekwa matumbawe; halafu, miti inachomwa. Baada ya kufanya hivi, fuatano la jambo ni kama katika Ureno.

Pamba yapatikana tele hapa. Namna yake ni nzuri na inapandwa na huota vizuri katika kisiwani. Manyoya ya kondoo si mazuri kuliko ya mbuzi. Watumwa huvaa nguo ya pamba kiunoni hufika chini mpaka miguu, na nyingine hutupwa juu ya mabega ambayo hufika chini mpaka pale nguo ya kwanza pamefungwa.

Sarafu zao za shaba nyekundu ni kama 'ceptis' zetu , nne kwa riali moja; sarafu za Ureno zinathaminishwa huko kama kadiri zathamanishwa nyumbani. Hakuna sarafu za dhahbu lakini uzito wa mithicali (8) yao ni sawa na reisi(9) 460 katika Ureno.

Kapitani-Mkuu alipita katikati ya mji mara mbili kutoka upande wa kwanza mpaka upande wa pili. Mara moja aliona swala shirini na tano walioachwa huru kisiwani. Pia, kuna mapaka wa witu wengi porini.

Kuna misikiti mingi ya matao, kama ile ya Cordova. Mamorisko wote wa cheo cha juu hushika tasbihi.

* Mfalme huyu labda alikuwa mtawala wa muda badala ya mfalme, Muhammad IV Ankony, (regent 1504-5) na Hajji 'Ali Hassan, (regent 1505-6). Ona KILWA :Masultani ya zamani;

Back to TOP


MOMBASA

Tarehe 9 ya Augusti meli ziliondoka Kilwa kwenda Mombasa, pita pwani kwa pwani juu ligi sitini. Meli ya Sam Rafael ilifika huko Augusti 14, lakini Kapitani-Mkuu alifika pamoja na meli nyingine kumi siku moja mapema.

Mamorisko wa Mombasa wamejenga pahali pa nguvu, pamoja na mizinga pale panapo mlango wa bandari, ambao ni mwembamba sana. Tulipoingia sisi, meli ya kwanza, iliyoamiriwa chini ya Gonzalo de Paiva, na aliyetangulia kutazamia mfereji, ilipigwa na bunduki kwa pande zote mbili. Mara moja, tulijibu mpigo huu wa bunduki, na tena kwa ukali hata baruti yao iliyokuwa ndani ya jengo lao ilishika moto. Ilianza kuwaka, na mamorisko walipokimbia, jamii ya manowari iliingia ndani na ilifunga nanga mbele wa mji. Siku ile ya mkesha wa sikukuu ya Kichukuzi(10), mji ulipigwa na makombora yote ya meli, wakati wote mizinga ya mji ilipojibia mioto yetu.

Aliposhuka nchini, Kapitani-Mkuu alikamata mmorisko mmoja ikawa alikuwa mmoja wa jumba la mfalme. Wareno walipata habari nzuri kwake.

Usiku wa kwanza jumla ya meli ilipofika Mombasa, alitoka pwani Mkristo Mhispania aliyekuwa alikaa kule, kazi yake mzingaji, na aliyebadilisha dini yake kuwa mwislamu. Yeye aliwaambia Wakristo waende zao, na Mombasa hauwi kama Kilwa; hawataipata mioyo ya watu yalikwe sawa na ya vifaranga, kama waliofanya Kilwa, lakini ingawa walikuwa na shauku ya kutua nchini watu walikuwa tayari kuanza kufanya kile kinachotakwa wale chakula cha usiku. Bali, Kapitani-Mkuu alisema atamsalimisha na atamsamehe, walakini yeye alikataa.

Mombasa ni mji mkubwa sana, na upo juu ya kisiwa cha ligi moja na nusu, au ligi mbili kwa kuzunguka. Mji umejengwa mwambani sehemu juu ya kisiwa, na hauna kuta upande wa bahari; ama upande wa nchi kavu, una kuta mrefu kama ngome. Vyumba ni aina moja sawa na vile vya Kilwa: viinginevyo vina ghorofa tatu na vyote vyapakwa na chokaa. Njia ziko nyembamba sana, na hata watu wawili bega kwa bega hawawezi kupita katikati humo: vyumba vyote vinavyo vyeti vya jiwe mbele barazani, na hivi njia zafanywa nyembamba zaidi.

Kapitani-Mkuu aliwakuta makapitanu wengine, na walipatana kuchoma mji usiku ule ule na kuuingia siku ya pili. Lakini, walipokwenda kuwasha mji walikaribishwa na mamorisko pamoja na mvua ya mishale na mawe. Mji una nyumba za kuzidi 600, zimeezekwa na makuti : haya yasanyikwa mabichi yakufaa kazi hii. Baina ya nyumba za jiwe, kuna nyumba za mibao zinazo kumbi na banda za ng'ombe. Kuna nyumba chache tu ambazo hazina vibanda vivi-hivi vimevyoungwa nazo.

Moto uliposhika, ulilipuka usiku kucha, na vyumba vyingi vilibomoka na mali ya kadiri kubwa sana iliharibika. Hiyo, kwa sababu kuna biashara huendeshwa katikati ya Sofala na Cambai(11) kwa bahari . Palikuwa meli tatu za Cambai na hata hizi hazikukimbia ukali wa shambulio. Usiku ulikuwa bila mwezi.

Siku ya 25 Augusti, sikukuu ya Kichukuzi cha Mama Mariamu, Kapitani-Mkuu alisimamisha meli nane upande mmoja wa Mombasa. Upande mwingine alikuwa mtoto wake, Dom Lourenqo d'Almeida. na meli tatu. Asubuhi ,mapema, walijiwekea tayari vifaa vyao na walifuturu. Kapitani-Mkuu alikuwa amekwisha toa amri marekibu yote yatelemke nchini wakati ule ule wakusikia mshindo wa mzinga mkubwa. Kwa hivyo, meli zote zilingoja tayari baharini; mara mshindo ukalia, wote walifanya bidii kushuka pwani kwa taratibu na vizuri. Wapigaji upinde na wapigaji mzinga walitangulia wote wengineo, wote wakapanda kigenge cha mpando kuingia mjini. Walipoingia, waliona baadhi ya nyumba zilikuwa hame kwa ajili ya moto wa usiku wa jana. Mbele zaidi walikuta nyumba za ghorofa tatu na walitupwa na mawe juu kwazo, lakini mawe haya yaliyokuwa yametupwa yalianguka juu ya kuta za njia nyembamba sana, na kwa hivyo nguvu za maanguko yao iliopotezwa. Pia,palikuwa roshani nyingi zilizotokea juu ya barabara na chini zao mtu aliweza kujihifadhia.

Kapitani-Mkuu alikwenda moja kwa moja kwa jumba la mfalme: alionyeshwa njia na mmorisko yule aliyekamatwa siku iliyotangulia. Alikuwa ametoa amri kwa wote wasiziingie nyumba nyoyote, na yoyote aliyefanya hivyo atakufa. Kapitani-Mkuu alipofika kasri, Kapitani Verraudez alipanda ukuta mara moja, na akalia wakati alipotweka bendera yetu: Ureno, Ureno. Na walikuwa mamorisko wengi waliouawa njiani wakati wakwenda kufika kule.

Walikuwa mamorisko karibu sitini wakaacha mji, wote katika nguo zao za majoho na vilemba; walikuwa wakaenda kusudia shamba la miti minazi, na hawakuonekana kama walikuwa na haraka. Wengineo walisema mfalme yuko miongoni mwao. Lakini, wakristo hawakufuata hawa. Wenyeji wote wa mji walichukuliwa kwa bustani hiyo ya minazi , na ingizo lake lililindwa na wapigaji upinde wa kuzidi 500. Hawa wapigaji upinde wote walikuwa watumwa wa mamorisko weupe, na walitii mabwana zao katika vifungo vyao kama wale wa Kilwa.

Kapitani-Mkuu alitoa amri ya kuteka mji na kila mtu achukue melini vyovyote amevyopatia; ili ifanywe mgawanyo wa nyara baadaye, mwishoni kila mtu apokee kigawanyo ya ishirini ya nyara zote. Sharti hilo hilo liliwekwa kwa dhahabu, fedha na lulu. Halafu, wote walianza kuteka mji na kutafuta vyumba, hata kuvunja milango wazi kwa kutumia mashoka na mitaimbo. Kulikuwa kiasi kubwa ya nguo za pamba mjini, zakwenda Sofala, kwa sababu pwani yote yapata nguo za pamba kutoka hapa. Hivyo, Kapitani-Mkuu alijipatia mwenyewe kigawanyo kizuri cha biashara ya Sofala. Zilichukuliwa nyingi za nguo ghali zilizokuwa zimetariziwa na hariri na dhahabu, na tele za zulia pia; kwazo moja iliyokuwa bila sawa katika uzuri wake, ilipelekwa kwa mfalme wa Ureno, pamoja na vinginevyo vyingi vya thamani.

Wakati wa usiku Kapitani-Mkuu alitoa amri watu wote waende shambani lililokuwa katikati ya mji na bahari. Vipande vya hilo viligawanywa, kila kapitani kipande chake, na kingojo kilishikwa. Walikuwa umbali wa mpigo wa bunduki kwa bustani ile palipokuwamo mamorisko pamoja na mfalme wao. Asubuhi ya tarehe 16, waliteka mji tena, lakini kwa sababu watu walikuwa wamechoka na ugomvi, na ukosefu wa usingizi, mali nyingi iliachwa nyuma hadi ila iliyoweza mtu kuibeba mwenyewe. Walichukua na vifaa, mchele, asali, siagi. ngamia wengi na ng'ombe wa idadi kubwa, tena na ndovu wawili. Walitembeza ndovu hawa katika uonyesho mbele ya wenyeji, kabla ya kwenda nao, kuwaogopisha. Walikuwa wafungwa wengi, hata wanawake weupe kwa watoto miongoni mwao, tena na matajiri waliokuwa watu wa Cambai.

Usiku wa Jumamosi, Kapitani-Mkuu alitoa amri wote warudi melini kwa utaratibu, na kujihadhari kuwatazamia mamorisko wakapoenda njiani. Wakristo walipotoka njia moja. ndiyo mamorisko waliingia njia nyingine kuangalia uharibifu uliofanyiwa, kwa sababu barabara na vyumba vilikuwa vimejazwa na watu maiti, na hao waliohesabikwa kama karibu 1,500.

Dom Fernandode Sà alijeruhiwa na mshale usiokuwa na ncha ya chembe; mingineyo ya mishale yao hutengenezwa na mti pamoja na chembe, ingine ya mti huchomwa na hulowekwa katika sumu ambayo haijulikani. Wengine wasema ni mti wenyewe unao sumu. Mishale inayo vyembe na majani nchani, hii ndio siyo hatari, kama ilivyokuwa dhahiri kwa hao waliokuwa wamejeruhiwa navyo.

Wasema mamorisko ambao mji huu ni mashuhuri zaidi kuliko mwingineo wote katika pwani ya Uhabshi. Kisiwa hiki kinazaa sana, na kinatoa vizao vya machungwa matamu, makomamanga, malimau na miwa; haya yote ni mengi hapa kuliko Kilwa.

Bunduki zote za mji zilipelekwa juu ya meli. Waliona mzinga mmoja wa zamani ulikuwa njiani, na watu watano hawakuweza kuuinua. Ilisemwa ulikuwa katika meli ya 'Rey' iliyopotewa karibuni. Nanga pia ilitafutwa, iliyokuwa imeibiwa kwa Amiri Vasco da Gama. Kwa sababu hawa wareno hawakuweza kuuchukua, waarabu walionyeshea huu kila mmoja mwingine. Wareno watano tu walikufa katika ugomvi, na wengi walijeruhiwa - zaidi kwa ajili ya Mungu kuliko kazi ya binadamu.

Baada ya kurudi vyomboni waling'oa nanga na walihama mpaka mapwa ya juu ili nanga zao zifunuke juu ya nchi kavu wakati wa kupwa maji. Walisimama huko siku kumi. Ilikuwa taabu mno kutoka katikati ya mlango wembamba, tena na mkabala wa pepo za nguvu halifu. Meli ya 'Lyomarda' ilipotea usukani wake na hawakuweza kuutafutia tena. Walilazimishwa watengeneze mpya na kila chombo kilitoa kwa kiingine kulabu moja kufanya kazi hii.

Chombo cha 'San Gabriel' kilifika tarehe 20 Augusti , mlingoti wake ulikuwa umevunjika, lakini mahali palipokuwa vyombo vya vifaa baado hakujulikana.

Sasa, mfalme wa Mombasa, na mfalme wa Malindi walikuwa kati ya ugomvi, na watu wengi walikuwa wameuawa kwa pande mbili zote. Sababu ya ugomvi ilikuwa urafiki wa mfalme wa Malindi pamoja na mfalme wa Ureno. Mwishoni, mfalme wa Mombasa alikuwa ameshindwa na mfalme wa Malindi, na wakati uliopo walikuwa rafiki. Kwa hiyo, mfalme wa Mombasa aliandika barua kwa mfalme wa Malindi :

" Mibaraka ya Mungu iwe juu yako,Sayyid Ali! Hii nikutaarifia kwamba amiri mkubwa amepita mjini, na ameuchoma na kuuteketea. Aliingia mji na nguvu kasi na ukali mno, na yeye hakuachilia mwanaume kwa mwanawake, ama mzee ama mtoto, na hata kitoto kidogo kabisa. Wale waliotoroka hawakuweza kukimbia ghadhabu yake. Hakuuwa wala kuchoma watu tu, lakini ndege uwinguni pia walipigwa na risasi. Uvundo wa maiti mjini una ukubwa hata siwezi kuingia kule; wala siwezi kupima mali wameyochukua nao kutoka mjini. Nakupa habari hizo za huzuni ili kukusalamini wewe mwenyewe."

Walikuwa watu wakuzidi 10,000 huko Mombasa, ambao 3,700 walikuwa na umri wa watu wajeshi.

Back to TOP


MALINDI

Kwa huko, walivuka bahari kwenda Malindi, ligi ishirini na tano zaidi kasikazini. Kabla ya ligi tano nje ya Malindi, walisimamishwa na mikondo ya nguvu, na hapa walikuta karaveli ya Johan Homere, aliyekamata visiwa viwili viwe chini ya utawala wa Ureno. Kimoja vivyo kilikuwa ligi 450 ng'ambo ya pili ya Rasi ya Taraja Zuri na kilikuwa bila watu. Walichukua kuni na maji kule.

Kingine kiko katikati ya Kilwa na Mombasa, na kinaitwa Zanzibar. Kwa sababu mamorisko wa kisiwa wamekwisha pata habari ya maangamizi ya Kilwa, walimpa kapitani vifaa na walisema wako tayari kuhudumu mfalme wa Ureno. Meli ilikuwa imekwisha fika kule tarehe 24 Augusti, na kuchukua maji, kuni na nyama. Mogadishu ndiko katika pwani hiyo hiyo na ni ligi 100 kutoka Malindi. Ni mji mkubwa ambao una farasi wengi........

Back to TOP


Notes: Maelezo.

  1. karaveli : aina ya chombo cha bahari. Tazama picha.Kusoma habari zaidi juu ya vyombo vya bahari vya Ureno wakati wa zamani hiyo tumia kiungo 'caravel'
  2. ligi:(league; pl; leagues). Kiasi ya umbali wa zamani, kila moja takriban maili tatu.
  3. mamorisko (moors) : jina lililopewa watu wa maghrebi au maberberi huko Ulaya.
  4. Al·mude.n.Kipimo cha maji - liquids -katika nchi nyingi. Ureno, almude ya Lisbon ni karibu 4.4; almude ya Oporto karibu 6.6, gallons; Uturki 'almud' ni karibu 1.4 gallons. [U. S.gallon ni kipimo karibu pishi mbili] [Pg. almude, or Sp. almud, a measure of grain or dry fruit, fr. Ar. al-mudd ; ÇáãÏ pl.ÇáÇãÏÇ a dry measure.Webster's 1913]
  5. hedera : Hedera Helix ; namna ya mti huku ulaya, katika kiingereza, ivy.
  6. berua : lami au katrani
  7. jozi : hasa walnut katika kiingereza.
  8. mithqal(kiarabu) : mawe ya kupima katika mizani, huko Misri, uzito wa 26 karati=3.68g.
  9. reisi(kireno) ; moja=riyali, sarafu ya Ureno; [Reis.n.Pg., pl. real, an ancient Portuguese coin.Webster's 1913]
  10. Kichukuzi:Sikukuu ya wakristo, hasa ya Mama Mariamu kuchukuliwa hewani baada ya kuacha dunia hii.
  11. Cambai :(pia, Canbay): Bandari kubwa ilikuwapo katika nchi ya Uhindi.

    The full English text of this extract from Hans Mayr's book can be found at Modern History Sourcebook

    • Asili ya chimbuko:E. Axelson, "South East Africa," 1940; pp. 231-238. G.S.P. Freeman-Grenville, The East African Coast: Selected Documents (London: Rex Collings, 1974), pp. 105-112.
    • Previously published source: E. Axelson, "South East Africa," 1940; pp. 231-238. Quoted in G.S.P. Freeman-Grenville, The East African Coast: Selected Documents (London: Rex Collings, 1974), pp. 105-112.


    Francisco de Almeida pia "Mkubwa Dom Francisco" (Uzazi: c.1450 AK/ K. 853 AH) , Lisbon; Ufo: March 1, 1510 AK/ 915 AH, Cape of Good Hope; Rasi ya Taraja Zuri, Afrika Kusini) alikuwa mheshimiwa, askari, na mvumbuaji wa Ureno. Alikuwa katika baraza ya Mfalme John II ya Ureno, na katika ugomvi kushindana na mamorisko, hata katika ushindi wa Granada, Uhispania. Aliacha Lisbon 1505 A.K / 960 A.H kwa hukumu ya Mfalme Manuel I ya Ureno, kama mjumbe wa utawala wa Uhindi wa kwanza wa Ureno, pamoja na vyombo 22 vya ugomvi baharini(armada) , karaki 14, na karaveli 6. Walipakia juu ya meli hizo jeshi la watu 1000 na 1,500.

    Wakatai wa kurudi, walifika Afrika Kusini na hapa walifunga nanga kuchukua maji. Baada ya biashara na urafiki pamoja na wenyeji (Wakhoikhoi), kulitokea matatizo, na wakhoikhoi walipoona nafasi ya shambulio wakapiga hawa hata Almeida mwenyewe, na watu wake 64, wakafa, miongoni mwao makapitani 11. Wakati wa mchana siku ile ile, baada ya kuongoa maiti wake alizikwa huko huko katika pwani ya mbele ya Cape Town.

    Rasi ya Taraja Zuri

    Bartholomew Diaz(c. 1450 - May 29, 1500) alikuwa msafiri wa kwanza kufika na kuzunguka upande wa kusini kabisa ya Afrika mwaka wa 1488 AK/ 892 AH. Wakati wa kurudi njia hii hii, alitaja rasi ya Afrika Kusini na jina la "Cabo das Tormentas", yaani "Rasi ya Tufani". Ilikuwa baadaye ambayo John II ya Ureno aliita rasi hiyo kwa jina la "Cabo da Boa Esperança", yaani "Rasi ya Taraja Zuri", au katika kiingereza "Cape of Good Hope".


    Left :

    Carrack/Karaki, aina moja ya meli 14 zilizotumikwa na Almeida katika safari yake

    Right :

    Caravela Redonda -aina ya karaveli ilyotumikwa na Almeida pamoja na tano nyingine

    Vasco da Gama (Uzazi: Sines Vidigueira, Alentejo, Portugal, c. 1469 AK/873AH; – Ufo: December 24, 1524 ; December 24, 1524 AK/ 930 AH ; Kochi, India) alikuwa msafiri maarufu, na mmoja aliyefaulu kuliko wengineo hata kuwa mtu wa kwanza kuvuka bahari kutoka Ulaya mpaka Uhindi. Aliacha Lisbon tarehe 8 July 1497 AK/ 902 AH na vyombo vya bahari vinne, ambavyo vilitajwa São Gabriel, meli ya aina ya karaki, São Rafael, kama ya São Gabriel, karaveli Berrio, na meli ya vifaa. Meli ya São Rafael labda ilikuwa ile ile iliyokuwa miongoni mwa marekibu ya Dom Francisco

    Back to Top


    Previous pageFull page ListNext page

    Zuru :Safari ya Kwanza ya Vasco da Gama

    © M. E. Kudrati, 2006:This document may be reproduced and redistributed, but only in its entirety and with full acknowledgement of its source and authorship