Mafundisho ya shule kwa mpangilio wa Kiislamu
“Uislamu ni tajiri sana kwenye upande wa elimu na hakuna elimu ambayo imeiacha.
Hivi karibuni tutatoa mwelekeo wa uislamu kwenye elimu, na tutanukuu maneno ya
Imaam Ghazali kwenye Ihyaa Uloomud-Diin. Tutatunukuu hapa sehemu ndogo kwa
kifupi sana, Imaam Ghazali anasema elimu imegawika kuwa lazima kwa kila mmoja,
na elimu iliyokuwa lazima kwa kikundi cha watu, elimu iliyokuwa makruuh na
elimu iliyokuwa mubaah na elimu iliyokuwa haramu.
Katika elimu iliyokuwa lazima, kasema si lazima mtu ajue milango yote ya
sheria bali ajue kila kinachotakiwa katika muda na hali alionao, akasema kwa
mfano si lazima kujua hukumu za Hijja kama hana uwezo na wakati wa Hijja
haujafika. Kisha akaendelea kueleza na akasema watu wanahangaika kusoma
maelezo ya undani wa sheria na mifano ya mas-ala ambayo hayatokei ila kwa
nadra na wakati mjini kwao hakuna daktari wa kike Muislamu wa kutibu wanawake
wa kiislamu, na ni jambo la lazima kwa wakazi wa mji na kama halijafanyika
wanapata madhambi wakazi wote.
Kwa hiyo ni wazi kuwa baadhi ya elimu tunazoziita za dunia ni lazima tujifunze
kwa amri ya dini yetu, na tusipofanya hivyo tutaingia kwenye madhambi makubwa.
Maelezo zaidi tutayatoa kwenye makala zetu zijazo.
Wajerumani walivyokuja Tanganyika, wakaona wasomi zaidi ni Waislamu, wanajua
kusoma na kuandika, wanajua hesabu na wanatumia tarakimu za kiarabu kwenye
maandiko yao, hata lugha ya Kiswahili ilikuwa wanatumia maandishi ya kiarabu.
Wakawaajiri hawa kwenye mahakama, na nafasi za Serikali.
Mwingereza alikuja na makusudio yake, ya kuuvunja uislamu na kuwadhoofisha
Waislamu, akajenga mashule na kuweka masharti anayetaka kujiunga lazima awe
mkristo, ili ajiunge, ndiyo wakati tuliopata majina ya Augostino Saidi na
mengineyo. Waliopenda dini yao, wakachukia masomo ya kizungu na kukataa
kupeleka watoto wao mashuleni, ili wasiwe wakristo, wakahifadhi dini yao,
lakini ikajijenga tabia ya kuchukia elimu za kizungu.
Kwa hakika elimu hizi si za kizungu, ni za Waislamu wenyewe na zinarudi kwao
wenyewe, Waislamu waliendeleza elimu na teknolojia, na wafalme wa kiislamu
waliwapa zawadi kubwa kubwa wasomi waliovumbua mashine mpya, na zawadi ya
kanisa ilikuwa ni kuwaua wanasayansi. Hapo ndipo wakazi wa nchi za kizungu
wakaamua kuweka mbali dini na sayansi & Teknolojia. Kitu hicho hakipo kwenye
Uislamu. Ndiyo elimu ya secular ilipoanza.
Tukirudi kwenye Tanganyika, nafasi za Serikali zikaanza kuchukuliwa na
wakristo, na wakaendelea kupata nafasi hizo, hadi Waislamu walivyoanzisha TANU,
hawakuwa na Muislamu wa kushika nafasi ya juu kabisa na kumweka mkristo kwenye
nafasi hiyo, na hatimaye wakristo wakaendelea kutawala.
Hiyo ni historia, tusiisahau, lakini pia isiwe ni sababu ya kutupia lawama
zote kwa historia, sisi tumefanya nini kuibadili historia hiyo? Waislamu bado
kwa asilimia kubwa sana wanachukia elimu za kizungu, na wana hiari wawasomeshe
madrasa tu, wasipate elimu za kizungu, au wawasomeshe elimu za kizungu na
wasipate elimu za dini, kama wanavyotoka Waislamu wengi hata kwenye shule
tunazoziita za Kiislamu. Hakuna sehemu ambapo tumeziweka hizi elimu za kizungu
ambazo kwa hakika si za kizungu ziendane na mafunzo ya Uislamu, na kama zipo
shule hizo labda hatuzijui.
Kwa kweli njia hizi mbili tumeziweka mbali sana, na hatujajenga njia ya
kuzikutanisha, Wanasayansi wakubwa wa kiislamu, wanaanza vitabu vyao kwa
Bismillahi, kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumswalia Mtume - Rehema na Amani
zimshukie - na bado wanabaki kuwa wanasayansi na wavumbuzi na wazungu wanaiba
uvumbuzi wao na kusema wamevumbua wao, bali kushika kwao dini kunawafanya wawe
wanasayansi wakubwa zaidi.
Nini cha kufanya ili tusomeshe na tusome hizi elimu za ki-secular, kwa mpango
wa kiislamu ???
-
Walimu Waislamu wa mashuleni wajitolee kuandika masomo ya shuleni bila
kubadilisha syllabus kwa mpango wa kiislamu. Kila Sura "chapter" iwe na utangulizi wa
aya za Qur-ani na Hadithi kuhusu Sura hiyo, na ndani ya Sura hiyo pia,
kuweko na aya ya Qur-ani na Hadithi. Sura hizo pia zitoe mchango wa
Waislamu kwenye somo hilo, bali kwenye kipengele hicho pia.
- Kuwe na masomo ya dini kwa uhakika wa masomo hayo. Masomo hayo ni kama
sheria ya Kiislamu, Sira, Tabia na mambo ambayo yanamuathiri Muislamu kila
siku. Isiwe kama shule zetu, tunamfundisha mtoto wetu jinsi ya kutoa hoja za
dini, jinsi ya kujibizana na kafiri na asiye na dini lakini ukimwuliza jinsi
ya kuswali, hajui, akienda chooni anajisafisha vipi, hajui. Wakati haya ndio
masuala muhimu zaidi kuliko kujua kutoa hoja.
- Walimu waambizane wenyewe kwa wenyewe umuhimu wa suala hili, walitangaze na kuliendeleza
suala hili, na kila mmoja afanye kilicho kwenye uwezo wake. Kila mtu afikishe
ujumbe kwa mwenziwe, mwenye elimu atoe mchango wa elimu, mwenye pesa atoe
mchango wa kuchapisha vitabu, mashule na kadhalika.
- Ikiwa tutasubiri mpaka tuunde Chama, Kamati, Jumuiya ambayo itashughulikia
suala hili, hatutafika popote. Tunajua udhaifu wetu, kila mmoja atakuja na
makusudio yake, wengine watakuja ili wajaze mifuko yao na matumbo yao, wengine
watakuja ili wapate umaarufu, na wengine watawekwa na vikundi ambavyo si vya
Waislamu ili waharibu hiyo Jumuiya na mwisho tutavunja Jumuiya yetu. Bora kila
mwenye uwezo afanye kilicho kwenye uwezo wake, na anayetaka mwongozo wa jinsi
ya kuandika vitabu vya mashuleni kwa mpangilio tuliotaja anaweza kutuandikia
(webmaster@uislamu.org) na Insha Allah tutamsaidia kiasi cha uwezo wetu. Pia
ambaye anataka kitabu chake kipitiwe, kisahihishwe, au hana uwezo wa
kuchapisha pia anaweza kutuandikia.
Mwenyezi Mungu atupe uwezo wote, wa
kuutumikia Uislamu na Waislamu kwa njia bora na ambayo anairidhia Yeye - Aamin.”
MWANDISHI: Makala hii imetolewa ikiwa ni sehemu ya maoni na imekusudiwa kuwa ni changamoto kwa umma, waalimu na wanafunzi wa Kiislamu. Imeandaliwa na Webmaster, www.uislamu.org. Mwenyezi Mungu amzidishie ya kheri juu ya kheri.
TAREHE: Jumamosi, 19 Aprili 2003.
Muhtasari huu umetayarishwa na Islamic Propagation Centre, S. L. P. 55105, Dar es salaam, Tanzania
|